Monday, 27 February 2017

SERIKALI YAISHUKURU AfDB KUKUBALI KUFADHILI MIRADI YA UJENZI WA BARABARA NA USAFIRISHAJI WA UMEME ILI KUFUNGUA KANDA YA MAGHARIBI

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kukubali kuendelea kufadhili miradi ya maendeleo ya kipaumbele hususani ya ujenzi wa barabara na usafirishaji wa umeme ili kufungua fursa za kiuchumi katika kanda ya Magharibi.
Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo alipokutana na Wakurugenzi Watendaji 12 wanaowakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kuanza mapema iwezekanavyo.
Amesema kuwa Benki hiyo iliahidi kutoa fedha ili kujenga barabara ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha lami na kwamba mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia kuchochea biashara ya wakazi wa maeneo hayo na Nchi jirani ya Burundi.
Pia mradi wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi huu utawezesha Mikoa ya ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na kufungua fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya  ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
“Katika kikao hicho tumewaeleza Wakurugenzi hao wa AfDB hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua katika kutatua changamoto ya Miundombinu ya Umeme na Barabara, kupanua fursa za Ajira, na kuharakisha maendeleo ya  ukuaji wa Sekta ya Kilimo ambayo inategemewa na wananchi wengi” Alifafanua Waziri Mpango.
Aidha amewaeleza wageni juu ya jitihada za Serikali ya Mhe. Dkt. John  Pombe Joseph Magufuli za kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, kupambana na rushwa na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Waziri Mpango ametumia fursa hiyo kuomba AfDB kusaidia kujenga uwezo wa Tanzania kukabiliana na majanga yakiwemo ya matetemeko ya ardhi, ajali kubwa za majini na kwenye migodi. Maeneo mengine ambayo AfDB imeombwa kuisaidia Tanzania ni uvunaji wa rasilimali za bahari (blue economy), kuelekeza mitaji katika Sekta ya kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameipongeza Benki ya AfDB kwa kuwa mdau mkubwa wa Maendeleo ya nchi za Afrika na hasa Tanzania kwa kuwa imekuwa mnufaika mkubwa wa program/ miradi inayofadhiliwa na  Benki hiyo.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wageni hao watakapokuwa wakitembelea miradi mbalimbali inayogharamiwa na AfDBi katika siku takribani tano ambazo watakuwepo nchini.
Kwa upande wa Wakurugenzi Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio ya kiuchumi kwa kuwa Tanzania imekuwa na viashiria vingi ambavyo vinaonesha uchumi wa Taifa ni imara ukilinganisha na nchi nyingine katika bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Aidha wameitaka Tanzania kuendeleza jitihada za kupambana na Umaskini hasa katika maeneo ya vijijini na kuongeza fursa za ajira ili kuharakisha maendeleo. Pia wameipongeza Serikali kwa mikakati waliyonayo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa  miaka mitano kwa kuwa unaendana na vipaumbele vya Benki hiyo.
Benki hiyo imeitaka pia Tanzania kushiriki na kuchangamkia fursa za miradi ya kikanda hasa katika Nishati ya Umeme, Barabara na Reli na pia kuhakikisha utawala bora. 

Sunday, 28 August 2016





Katibu Mkuu Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Natalia Kanem amesema vijana 500 millioni kote duniani (25%) wanaishi katika familia Masikini huku Afrika ikiwa na idadi kubwa zaidi.
Kanem alisema hayo jana katika maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Zakheim Mbagala na kauli mbiu ikiwa ni “Tokomeza umasikini kwa uzalishaji endelevu na matumizi yenye tija”.
“Watu 2 billioni Duniani kote ni vijana wengi wameshindwa kufanikiwa katika ndoto zao kutokana na changamoto zinazofanana, na kauli mbiu hii inagusa uhalisia unaoweza kuwafikisha katika mafanikio vijana wa Tanzania, Afrika na Dunia nzima”, alisema Kanem.
Kanem aliongeza kuwa vijana ni nguvu kazi na ni mhimu kwa maendeleo ya Taifa hivyo katika safari yao ya kuelekea utu uzima na uzee  sasa ni muda wa kujitathimini wao ni wakina nani, ni zipi haswa ni ndoto zao na kutafta fursa ili waweze kuzifanikisha.
Hata hivyo vijana waliohudhuria walitoa tamko na maombi kwa Serikali ili waweza kuzishinda changamo zinazosababisha kukwama kwa mafanikio yao.
Muwakilishi wa vijana Dickson Goerge alisema Serikali haina budi kuboresha Sekta ya Elimu kwa ujumla wake, Sekta ya Afya, kuweka nafasi za vijana katika uwakilishi wa ngazi za juu, Kupiga vita Rushwa, Kuasimamia kanuni za Utawala Bora, Usimamizi mzuri wa Rasilimali za Taifa na kuwapatia vijana fursa za ajira.
“Vijana tunahitaji mfuko wa Taifa kwaajili ya kutuwezesha katika mambo yetu, tunahitaji usimamizi mzuri wa rasilimali za Taifa hususani mbuga na madini, Uwepo wa fursa za ajira, tunahitaji maboresho katika sekta ya afya kuwe  na bima ya matibabu kwaajili yetu ili sasa tuweze kupambana na umasikini na kuongeza uzalishaji katika Taifa letu”, alisema George.
Mratibu wa progrmu ya kuendeleza  ujasiliamali kwa vijana Noreen Toroka kutoka Shirika la kazi la Umoja wa mataifa (ILO) alisema Serikali ya Tanzania ipo katika mpango wa kuelekea katika nchi ya viwanda lakini vijana ambao ndiyo chachu katika kufanikisha hilo bado wanachangamoto nyingi ikiwa ni pamoja na Ukosefu wa ajira na umasikin.
“Licha ya kwamba ripoti ya hivi karibuni inaonesha kupungua kwa tatizo la ajira kwa asilimia 2 kutoka asilimia 13 mwaka 2006 - aslimia 11 mwaka 2015 bado kuna uhitaji mkubwa kwani ajira kwa vijana inaweza hata kuboresha sekta nyingine ikiwemo ya afya”, alisema Toroka.

Aidha kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa Bam-Ki-Moon kuhusu siku ya vijana mwaka huu inaelezea changamoto ambazo zinakwamisha mafanikio ya vijana kuwa ni Umasikini, Kushindwa kumiliki mali, Njaa, Upotezaji wa Chakula, , kushindwa kunufaika na rasilimali za nchi zao na  uharibifu wa mazingira unatokana na viwanda.
“Ukiwekeza katika vijana wanachangia katika upatikanaji wa masoko mapya, soko huria, makazi endelevu, usafiri endelevu na mengine mengi yanayowanufaisha watu na Dunia kwa ujumla”, alisema Bam Ki-Moon.
Aidha Moon alitoa wito kwa vijana wote Duniani kushiriki kikamilifu katika kufanikisha malengo endelevu ya Dunia kulingana na mahitaji ya Serikali za nchi zao.